. UCHAWI
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la 3, neno ‘uchawi’ limefafanuliwa katika sehemu kuu mbili zifuatazo, Kwanza ni ‘ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalum vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe; au juju. Pili ni ‘vifaa vinavyotumika katika shughuli za kurogea’
Neno “mchawi’ limetafsiriwa kuwa ni mtu anayesadikiwa kuwa anaweza kuwadhuhuru watu kwa kuwaroga; mlozi, kahini. Wachawi mara nyingi hufanya kazi katika ulimwengu wa roho yaani ulimwengu ambao huwezi kuuona kwa macho ya kimwili.
Kwa mujibu wa Merriam-Webster dictionary neno “witchcraft” ambalo katika Kiswahili hutafsiriwa kama “uchawi” limetafsiriwa kama “magical things that are done by witches, or the use of magical powers obtained especially from evil spirits” kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili “uchawi” maana yake mambo ya kimiujiza yanayofanywa na wachawi”, maana ya pili, “matumizi ya nguvu za kiroho zilizochukuliwa toka kwa roho waovu”. Wengine wanatafsiri uchawi kama matumizi ya silaha za mashetani au nguvu za mashetani ili kusababisha madhara kwa watu.
Iyke Nathan Uzorma, Katika Kitabu chake kinachoitwa “Mkuu Wa Wachawi Sasa Ampokea Kristo” anaandika hivi; mchawi ni mwanadamu ambaye hupitia vitengo mbali mbali katika ufalme wa giza, ili atumiwe kuzidhihirisha nguvu zisizoonekana za Shetani katika Ulimwengu wa mwili. Kwa lugha nyingine mwanadamu yeyote ambaye hutumia nguvu au maarifa yasiyoonekana kudhuru, kuharibu, kudhibiti, kumiliki, au kupumbaza akili za mwanadamu mwenzake huyo ni mchawi.
Tofauti kati ya Ushirikinana Uchawi
Yapo mahusiano kati ya wachawi na waganga hasa waaguzi, wapiga bao na wanaosoma nyota na washirikina. Mwangalizi mkuu wa WAPO Mission International askofu Sylvester Gamanywa katika makala yake “ongezeko la hofu ya uchawi makanisani” iliyochapishwa katika mtandao wa gospelkitaa.co.tz anasema Kuna makundi mawili yenye kushughulika na uchawi.
a) Kundi la kwanza ni la “washirikina” yaani jamii ya watu wanaoamini mambo ya uchawi na mizimu. Hili ni la “washirikina” ambao ni wateja wa “waganga wa tunguri” wenye kudai kutoa kinga na tiba dhidi ya uchawi.
b) Kundi la pili, ni jamii ya “wachawi wenyewe” wenye ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalum vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe, au juju nk. Kimtazamo, “mchawi” ni tofauti na “mshirikina” kwa kuwa “mchawi” ni “bingwa wa kuloga” wengine; na “mshirikina” ni “mteja wa mganga” anayetafuta msaada wa kinga au tiba dhidi ya uchawi. Kivitengo vya kiitikadi, wachawi ndio “viongozi wa kiroho” katika uchawi; wakati “washirikina” wao ni “waumini wanaosalishwa kwenye ibada za kichawi”. Kibiblia, uchawi, uganga watunguri na ushirikina vyote ni idara moja ya uchawi na wahusika wote ni wafungwa wa majini na mizimu na majeshi ya pepo wachafu.
Makundi manne ya wachawi kulingana na walivyoingia katika uchawi
a) Kundi la kwanza, walioingia kwa kurithi, wapo watoto wengi wanao zaliwa kwenye familia ambazo kuna mambo ya uchawi, na wanaingizwa katika shughuli za uchawi tangu wakiwa matumboni mwa mama zao. Katika huduma yangu nimekutana na watoto wadogo kabisa wa mwaka mmoja, wengine hata miezi miwili tu wakiwa tayari ni wachawi. Si unakumbuka Yohana Mbatizaji alijazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake, kabla hajazaliwa, na katengwa kwa kusudi maalumu la Mungu katika dunia hii (Luka 1:15). Usishangae kusikia Shetani amemjaza mtoto mdogo aliyopo tumboni mwa mama yake roho ya uchawi kabla hajazaliwa na mara nyingi watoto hawa huwa umilikiwa na mapepo kwa kibali maalumu toka kwa wazazi wake
b) Kundi la pili, walioingia katika uchawi na watu wengine kwa kulazimishwa, wapo watoto wengi na watu wazima waliochukuliwa na kuingizwa katika uchawi na hata wanapotaka kutoka ni vigumu kwao. Namna wanavyoingizwa katika uchawi inatofautiana mtu na mtu, nimeshuhudia watoto wadogo wakiwa wameingizwa katika uchawi na watoto wenzao baada tu ya kupewa vyakula kama vile maandazi, pipi, biskuti na kadhalika. Wengine walijikuta tu wapo kwenye Ulimwengu mwingine bila kujua waliendaje na baadaye wanajikuta wanapewa maelekezo ya kazi, pamoja na kurishwa viapo vya kuto kutoa siri na utii pindi unapo agizwa katika kazi yoyote ile. Kundi hili hufanya shughuli za uchawi kwa kushurutishwa na wanapojaribu kutaka kutoka vitisho na mateso huzidishwa. Watu wa kundi hili wanafanya shughuli za uchawi kwa shingo upande. Tumekutana na watu wa mtindo huo mara nyingi katika huduma.
c) Kundi la tatu, walioingia kwa hiari yao wenyewe, lipo kundi kubwa la watu ambao wameingia katika uchawi kwa hiari yao wenyewe kabisa, katika mikoa ya Pwani ya bahari ya Hindi si ajabu kusikia wapo watu ambao wanakwenda kununua majini ya uchawi kwa lengo la kupambana na maadui zao. Lakini pia inasadikika wapo watumishi wa Mungu ambao walianza vizuri, lakini kwa sababu ya tamaa ya pesa, na nguvu za miujiza wanaamua kuzigeukia nguvu za uchawi.
d) Kundi la nne, walioingia bila kujua, aidha na watu wengine, au walijiingiza wenyewe pasipo kujua wanaingia katika jamii ya wachawi na hawajui kama wanatumika katika shughuli za uchawi (blind witches), Nakumbuka tuliwahi kufanya huduma ya binti mmoja ambaye alikuwa anashiriki katika shughuli za uchawi bila ya yeye kujua, baadae akaanza kusumbuliwa na maumivu makali ya kichwa kwa sababu alihamia nyumba ya wana maombi kama mfanyakazi wa ndani, tulipoingia katika huduma na yeye tulishitushwa kusikia kuwa binti yule alikuwa mchawi pasipo yeye kujua, asante Yesu kwasababu alifunguliwa na kuwekwa huru. Siku kadhaa baada ya huduma, nilkaa na yule binti kumuuliza mambo mawili matatu yaliyojitokeza katika huduma. Yule binti akaniambia mara nyingi alikuwa akiota ndoto yupo na kundi kubwa la watu asio wafahamu, na huko anajiona ancheza ngoma mbali mbali, anapika na kula nyama na vyakula mbali mbali. Na anapoamka asubuhi anajikuta kashiba, tumbo limejaa kabasa. Alikuwa mchawi aliyeingizwa na ndugu zake wa karibu kabisa pasipo yeye mwenyewe kujua.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni